BAADA ya kukomba pointi tatu kwenye mchezo ulipita dhidi ya Dodoma Jiji, Septemba 29 2024 kikosi cha Simba leo kinatarajiwa kuwa na kazi ya kusaka pointi tatu dhidi ya Coastal Union mchezo unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa KMC, Mwenge.
Ikumbukwe kwamba kwenye mchezo huo bao pekee la ushindi kwa Simba lilifungwa na Jean Ahoua dakika ya 63 ni bao lake la pili ndani ya ligi msimu wa 2024/25 bao la kwanza alifunga kwenye mchezo dhidi ya Fountain Gate na kwenye mchezo huo alitwaa tuzo ya mchezaji bora.
Pointi za Simba kibindoni ni 12 baada ya kucheza mechi nne ikiwa nafasi ya 3 huku safu ya ushambuliaji ikiwa imetupia mabao 10 inakutana na Coastal Union yenye pointi nne baada ya kucheza mechi 6 ikiwa nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi ambao vinara ni Singida Black Stars wenye pointi 13 kibindoni ni mechi 5 wamecheza, ushindi katika mechi nne na sare mchezo mmoja.
Fadlu Davids, Kocha Mkuu wa Simba ameweka wazi kuwa mchezo wa leo utakuwa mgumu kutokana na mpinzani wao kuwa imara lakini wataingia kwa mpango wa kutafuta ushindi.
“Unajua kucheza mechi za ushindani kinachohitajika ni pointi tatu muhimu hivyo tupo tayari na makosa ya mechi zetu zilizopita tumefanyia kazi kikubwa ni kuona kwamba tunapata ushindi licha ya ushindani uliopo kwa kuwa haitakuwa rahisi ipo wazi.”