Pacome Zouzoua

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua amesema wana kazi kubwa ya kufanya ili kupata ushindi kwa namna yoyote ile dhidi ya CR Belouizdad. Lakini amekiri ubora wa kikosi chao kuwa na mwendelezo mzuri kwenye michuano yote.

Pacome ambaye amepachika mabao sita na asisti tatu kwenye ligi huku akifunga matatu Ligi ya Mabingwa, amesema ushindi mfululizo kwenye mechi tatu za ligi hauwezi kuwavimbisha vichwa kwa kuamini kuwa watakuwa na mchezo rahisi, lakini watapambana kama fainali.

“Tunahitaji kufanya maandalizi ya kutosha bila kuangalia matokeo yaliyopita na mchezo wetu na CR Belouizdad ni muhimu ndio utatupa picha ya sisi kutinga hatua inayofuata,” alisema staa huyo ambaye Yanga jana iliita siku hiyo ya Jumamosi kuwa “Pacome Day”.

“Mchezo wa Jumamosi ni fainali, kila upande, kila kwenye kundi letu ‘Kundi D’ timu ina nafasi ya kutinga hatua ya robo fainali, hivyo kilichobaki kila mmoja ashinde mechi zake tukutane mwisho wa mechi za makundi,” alisema staa huyo wa zamani wa Asec ambayo tayari imeshafuzu robo.

Pacome ambaye amefanya vizuri kwenye mechi zote za makundi, alisema kama wachezaji wanatambua umuhimu wa mchezo huo na watafanya kila litakalowezekana ili waweze kufikia lengo la kuhakikisha wanaandika rekodi nyingine ya kutinga robo fainali kwenye michuano hiyo mikubwa zaidi Afrika.

“Benchi la ufundi linafanya kazi vizuri na sisi kama wachezaji tunazingatia kile tunachoelekezwa kwa lengo moja la kupata matokeo ya ushindi ili kuweza kutafuta rekodi nyingine baada ya makundi,” alisema.

Akizungumzia ubora wake na kikosi kwa ujumla, alipongeza benchi la ufundi kuwa na programu nzuri licha ya timu kucheza mechi mfululizo kwani wamekuwa na mfululizo wa ubora, huku akitaja siri kuwa wana benchi la ufundi zuri.

“Timu yetu inafanya kazi kwa kushirikiana kuanzia kocha wa makipa, viungo na kocha mkuu wamekuwa na nia nzuri na sisi, kutujenga kisaikolojia kabla ya mchezo na kutuandaa vizuri.

“Tunacheza mechi leo, tukimaliza jioni au asubuhi tunafanya mazoezi ya kurudisha utimamu wa mwili. Hii inasaidia kuona wachezaji wanakuwa na kasi na pumzi nzuri,” alisema.

Akijizungumzia, Pacome alisema ubora wake unatokana na kucheza timu moja na wachezaji ambao wana uwezo mzuri na wanaelewana uwanjani.

“Nipo kwenye timu bora iliyosheheni vipaji na wachezaji wapambanaji hii inanipa wakati mzuri wa kupambana na kufanya kile kinachowapa nguvu ninaocheza nao,” alisema.

5 ZILIZOPITA
KMC 0-3 Yanga
Prisons 1-2 Yanga
Yanga 2-1 Mashujaa
Yanga 1-0 Dodoma
Kagera 0-0 Yanga

CR 0-0 Ahly
CR 2-0 Souf
Bayadh 2-1 CR
CR 2-0 Oran
CR 3-1 JS Soura

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YA SOKALEO, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here