Kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amesema licha ya kuondolewa mapema katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, anaamini timu hiyo ina kikosi bora chenye ushindani na nafasi yao mwisho wa msimu kwenye ligi iko palepale.
“Hakuna mchezaji ambaye alitamani tuishie njiani, tulikuwa na malengo makubwa lakini imeshatokea, hatujakata tamaa, tutapambana kuhakikisha tunaipata tena nafasi hiyo msimu ujao na hilo linawezekana kwa sababu tuna kikosi kizuri,” alisema na kuongeza:
“Hata timu ambazo zimekuwa zikifika mbali zilianza kama sisi na kuna timu licha ya ukongwe wao kwa kushiriki michuano hiyo hazijawahi kutwaa mataji, hivyo mwanzo ni mgumu, naamini tukirudi tena hatuwezi kurudia makosa.” Fei Toto alisema makosa machache waliyoyafanya ndio yamewaondoa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa, sasa wanarudi kupambana katika Ligi Kuu wakidhamiria kutwaa taji hilo na Kombe la Shirikisho.