UONGOZI wa Singida Black Stars umeweka wazi kuwa malengo makubwa ni kuleta ushindani kitaifa kutokana na usajili makini waliofanya pamoja na uzi mzuri kuliko timu zote Bongo kuwa mali yao kwa msimu wa 2024/25.
Timu hiyo inanolewa na Kocha Mkuu, Patrick Aussems wengi hupenda kumuita Uchebe aliwahi kuifundisha Simba inayoshiriki Ligi Kuu Bara na mafanikio yake makubwa akiwa na timu hiyo ilitinga hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ipo wazi kwamba Agosti 10 ilikuwa ni Big Day moja ya tamasha kubwa maalumu kwa utambulisjo wa wachezaji wapya kuelekea msimu wa 2024/25 pamoja na wale waliokuwa na kikosi hicho kwa msimu wa 2023/24.
Kwenye tamasha hilo Singida Black Stars ilicheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Aigle Noir ya Burundi ambayo kocha msaidizi ni Amiss Tambwe aliyewahi kucheza Yanga na Simba kwa nyakati tofauti ilipata ushindi wa bao 1-0 likifungwa na Joseph Guede ambaye ni ingizo jipya ndani ya timu hiyo.
Hussen Masanza Ofisa Habari wa Singida Black Stars ameweka wazi kuwa malengo makubwa ni kuwa na matokeo bora kwenye mechi za ushindani na wapo tayari kufanya vizuri kitaifa.
“Baada ya kukamilisha utambulisho wa wachezaji, benchi la ufundi kwenye tamasha kubwa na lenye mvuto Bongo la Big Day sasa tunakwenda kuhamishia nguvu kwenye mechi za ushindani hilo lipo wazi kwani wachezaji wapo tayari na tunaamini itakuwa hivyo mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi.
“Tuna uzi mzuri na mkali kuliko wote Bongo hilo lipo wazi na unapatikana kwenye maduka yote, mashabiki wetu wajipatie uzi mzuri ambao unavutia. Kwenye upande wa jezi hatujawahi kufeli tupo vizuri na uwanjani pia tutakuwa imara.”