WAKATI tetesi zikieleza kuwa Kibu Dennis kagomea kuongeza dili jipya ndani ya timu hiyo akiwa na ofa zaidi ya tatu mezani kimtindo uongozi wa Simba umejibu hoja hiyo.
Ipo wazi kwamba Kibu ni chaguo la kwanza la makocha wote ambao wamepita Simba ikiwa ni Robert Oliveira, Abdelhakh Benchikha na sasa Juma Mgunda.
Kibu anatajwa kuwa kwenye rada za mabosi wa Azam FC na Yanga ambao wanahitaji saini ya kiungo huyo mshambuliaji mwenye bao moja na pasi tatu za mabao.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally, amesema kuwa: “Licha ya timu kutajwa kuwa mbovu lakini wachezaji wake wanatajwa kuhitajika katika timu nyingine. Mchezaji tunayemtaka atabaki.”
Msimu wa 2023/24 ndani ya Ligi Kuu Bara mwamba huyo ametoa pasi tatu za mabao na kufunga bao moja ambapo huenda akakosekana kwenye mchezo wa leo dhidi ya Mtibwa Sugar.
Simba iliyotoka kulazimisha sare ya kufungana mabao 2-2 dhidi ya Namungo ina kibarua cha kusaka pointi dhidi ya Mtibwa Sugar, Mei 3 Uwanja wa Azam Complex.