KOCHA Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema kwamba michezo ya Ngao ya Jamii inaongeza ubora zadi kwa Kikosi chake, na haswa mechi dhidi ya Simba na Azam FC.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Gamondi, alisema mchezo dhidi ya Simba na huu wa leo unakisaidia kikosi chake kuimarika kutokana na ugumu na ubora wa wapinzani wao.
Alisema anatarajia kukutana na mchezo mgumu mbele ya Azam kwa wapinzani wao hao ni timu nzuri na anaiheshimu.
“Kwa upande wangu ninafurahi kukutana na timu yenye ushindani kama Azam FC kwa kuwa inakifanya kikosi changu kizidi kuwa bora zaidi, ninaomba mashabiki wetu waje kwa wingi uwanjani kuangalia burudani tutakayowapa,” alisema Gamondi.
Alisema makosa madogo madogo aliyoyabaini katika mchezo wao wa nusu fainali dhidi ya Simba ameyafanyia kazi ili yasiweze kujirudia kwenye mchezo leo.
Kwa upande wake Dickson Job ambaye alizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake alisema mchezo huo utakuwa na upinzani kutokana na timu zote kuwa na mabenchi bora ya ufundi.
” Sisi wachezaji tunafahamu mchezo huo utakuwa mgumu hivyo tunaahidi kupambana ili tuweze kupata matokeo mazuri, alisema Job.
Kwa upande wake, Kocha wa Azam, Ferry alisema wanatarajia kupata ugumu mbele ya wapinzani wao kwa kuwa ni timu inayofanya vizuri kwa sasa.
“Mchezo utakuwa mgumu sitaki kuzungumzia Yanga kwa kuwa hakuna mtu asiyefahamu ubora wake, kikubwa ni kupata ushindi,” alisema Ferry.
Alisema wamejiandaa na wapo tayari kukutana na yanga kwenye mchezo huo wa leo.