YANGA WAMEJIPANGA KUFANYA MAKUBWA KIMATAIFA
UONGOZI wa Yanga umeweka wazi kuwa kutokana na maandalizi ambayo wanayafanya hesabu kubwa ni kufanya kweli kuelekea mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ambao ni hatua ya robo fainali.
Chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi Yanga imetinga hatua ya robo fainali ikiwa na pointi 8 ambapo katika Kundi D ilikuwa pamoja na Al Ahly ya Misiri hawa mchezo wa kwanza walitoshana nguvu Uwanja wa Mkapa na ule wa pili, Yanga ilipoteza.
Ipo wazi kwamba Tanzania katika hatua hii ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali ina timu mbili, Yanga pamoja na Simba itakayocheza na Al Ahly mchezo wao unatarajiwa kuchezwa Machi 29 Uwanja wa Mkapa.
Mchezo wa Yanga dhidi ya Mamelod unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa Machi 30 huku maandalizi kwa Yanga yakiwa yameshaanza kuelekea mchezo huo muhimu unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amesema kuw wanatambua umuhimu wa mchezo huo watawashangaza wengi wanaowabeza baada ya kupangiwa Mamelodi Sundowns.
“Kuelekea mchezo wetu dhidi ya Mamelod nina amini kwamba tutawashangaza wengi kwa kuwa wanaamini hatutaweza kufanya vizuri lakini imani yetu ni kuona tunapata matokeo na kuendelea kufanya vizuri kwenye mechi za kimataifa inawezekana mashabiki wa Yanga tuzidi kuwa pamoja,”.