Pacome Zouzoua, Max Nzengeli na Yao Kouassi ni miongoni mwa majina makubwa Yanga kwa sasa. Licha ya usajili wao (wa kimataifa) kuwa wa kawaida kutokana na wengi kutowajua walikotoka, lakini viwango vyao vimewabeba na kutajwa ndio wanaoibeba Yanga kwa sasa. Katika usajili wa wakati huo, moja ya majina yaliyotua ni Gift Fred.

Beki huyu wa kati wa kimataifa wa Uganda, tofauti na matarajio ya wengi baada ya kuimbwa kwenye usajili wake, hadi sasa hajaonyesha kiwango bora kutokana na kukosa namba kikosini.

Kwenye tetesi za usajili za dirisha dogo lililopita, jina lake lilikuwa miongoni mwa watakaoachwa. Hata hivyo, licha ya dirisha lijalo kubwa mwisho wa msimu pia kuhusishwa ataondoka, lakini kuna uwezekano akaendelea kuwepo.

Sababu kubwa ni kiwango alichoanza kukionyesha tangu kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024. Hata mchezo wa juzi Jumanne wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports Federation Cup dhidi ya Housang FC Yanga ikishinda mabao 5-1, alionyesha kiwango safi. Pengine kiwango kitaongezeka katika michuano ijayo ambayo chama lake linashiriki.

Alisajiliwa akitokea Sports Club Villa ya nchini kwao alikocheza kuanzia 2021 hadi 2023. Alikulia kwenye akademi ya Chuo Kikuu cha Bugema, Uganda na mwaka 2019 alibeba tuzo ya beki bora wa mashindano ya vyuo vikuu.

Baada ya kufanya vizuri kwenye mashindano hayo mwaka 2020 alisajiliwa na Gomba Lions na kutwaa Kombe la Masaza Cup, akichaguliwa kuwa beki bora, kabla ya kunaswa na Villa.

Ni wazi ameanza kuonyesha kiwango Yanga na hapa Mwanaspoti linakuletea mambo yatakayombeba beki huyo na kuendelea kuvaa jezi ya Wananchi msimu ujao.

NAFASI KIKOSINI

Ingawa namba zake alikotoka hazidanganyi, kwenye kikosi cha Ynaga nafasi yake imekuwa finyu. Hii ni kutokana na uwepo wa mabeki wazawa Bakar Mwamnyeto, Ibrahim Bacca na Dickson Job ambao waliifikisha salama timu hiyo katika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita.

Mabeki hao sio tu tishio Yanga, bali hata kwenye timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kwenye michuano ya kimataifa.

Wamekuwa wakibadilishana namba na hilo limempa wakati mgumu Gift wa kucheza na amekuwa akiingia mara moja moja kikosini na kwenye Ligi Kuu Bara amecheza dakika 21 tu.

Katika dakika hizo beki huyo amecheza mechi 10, ikiwa ni dakika tano dhidi ya Geita Gold – timu yake ikishinda mabao 3-0 kisha dakika 16 dhidi Mtibwa Sugar na Yanga ilishinda mabao 4-1.

Pamoja na nafasi zingine anazoweza kupata msimu huu na kufanya vizuri ikiwamo juzi alipocheza kwa dakika 90 katika mechi ya Kombe la Shirikisho, hii inaweza kuwa sababu mojawapo ya Yanga kuendelea naye kikosini kwa sababu kama mabeki wawili wakiumia kocha atalazimika kumtumia.

NIDHAMU

Ilikuwa ni ngumu kumchambua beki huyo kutokana na kutomfahamu vizuri na uchache wa nafasi alizocheza. Kadi nyingi zimekuwa zikitoka kwa mabeki na viungo kutokana na kazi wanazofanya kuwazuia wapinzaji wasifike langoni, lakini Gift ameonyesha kitu tofauti.

Katika dakika 270 alizocheza kwenye Kombe la Mapinduzi kule Zanzibar imeonyesha namna anavyoweza kukaba na kuzuia timu pinzani kwa nidhamu alikofanikiwa kuondoka na tuzo mbili za mchezaji mwenye nidhamu licha ya timu yake kutolewa kwenye robo fainali.

Alipokuwa Villa msimu wa kwanza 2021/22 Gift alicheza mechi 26, akifunga mabao mawili, kadi ya njano moja na hakupa nyekundu. Msimu uliofuata alicheza michezo 27 akifunga mabao mawili, akapata kadi za njano mbili na kumaliza bila nyekundu.

KIMO KINAMBEBA

Sifa kubwa aliyonayo beki huyo mwenye ni kasi, nguvu, maarifa na nidhamu ni pamoja na urefu alionao.

Ukiangalia safu ya ulinzi ya Yanga ni Mwamnyeto ambaye ni mrefu tofauti na Job na Bacca ambao vimo vyao ni vya kati.

Mganda huyo ana urefu wa mita futi 6.1 na umbo ambalo linamuwezesha kukabiliana vyema na mastraika.

Faida nyingine ni urefu alionao unamfanya kukabiliana vyema na mipira mirefu ya wapinzani kwenye eneo analocheza.

WASIKIE WADAU

Akimzungumzia beki huyo, Kocha wa zamani wa JKT, Mashujaa na Azam, Abdul Mingange anasema kwa levo iliyopo Yanga kwa sasa haihitaji kumsubiri beki aina ya Gift.

Anasema beki huyo hawezi kuisaidia kuanzia Ligi Kuu hadi kimataifa kutokana na Mwamnyeto, Bacca na Job kushika vyema nafasi hiyo.

“Sijui kwa sababu ni mashindano ya Mapinduzi, lakini nilivyomuona hana spidi,” anasema Mingange.

Winga wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Dua Said anasema Yanga inatakiwa kumpa nafasi ya kucheza kwenye ligi ili ipate kumjua vizuri kama ilivyo kwa Bacca ambaye sasa ni tegemeo.

Dua anasema haoni kama ni mchezaji mbaya kwa kuwa beki huyo akipangwa na wachezaji ambao hawana uzoefu huwa na kazi ya kusahihisha makosa ya wenzake.

“Labda kama kocha ameona upungufu mwingine, lakini kwangu anafaa kabisa na ana sifa za kuwa beki wa kati kuanzia kimo. Hatujamuona sana naamini Yanga ataleta ushindani kwa wenzake kama atapewa muda mwingi,” anasema Dua.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YA SOKALEO, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here