Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Saimon Msuva mwenye miaka 30, ameonja kwa mara nyingine utamu wa Ligi Daraja la Kwanza nchini Saudia Arabia, lakini jambo la kufurahisha ni kubebeshwa msala wa Mgambia Ousmane Barry ambaye ndiye aliyekuwa akiongoza safu ya ushambuliaji ya timu ya Al-Najma.

Msuva ameonja utamu huo kwa kucheza dakika 90 wakati Al-Najma ikiwa ugenini ambako ilitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Ohod Club na kuambulia pointi moja ambayo imeifanya kuwa katika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Daraja la Kwanza kati ya timu 18 ikiwa na pointi 20.

Pamoja na ugeni wake, Msuva alianza katika mchezo huo na kubebeshwa majukumu ya Ousmane ambaye amejiunga na Al-Ula ya Ligi Daraja la Pili nchini humo mwezi uliopita. Nyota huyo ameondoka Al-Najma akiongoza orodha ya wafumania nyavu kwenye ligi hiyo akiwa na mabao 13.

Licha ya kwamba hakufunga wala kutoa asisti, Msuva alitumika kama mshambuliaji wa mwisho (namba tisa) katika eneo ambalo awali alikuwa akicheza kwenye ligi hiyo wakati akiwa na Al-Qadsiah ambayo kwa sasa ndio inayoongoza msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 41 baada ya michezo 20 kuchezwa.

Akizungumza kwa simu, Msuva amesema mabao yatakuja tu na ni suala la muda kwake, lakini ambacho anapambana ni kuzoeana kwa haraka na wachezaji wenzake kwenye kikosi hicho ili kufanikisha mipango ya timu.

“Nina furaha sana kupata nafasi ya kucheza mchezo wangu wa kwanza na timu yangu mpya. Ujue kuna kitu kwangu waliona ndio maana wakanisajili na mimi sipo tayari kuwaangusha,” amesema mchezaji huyo na kuongeza:

“Napambana kuendana na wenzangu. Hii ni hatua ya kawaida kwa mchezaji yeyote mpya. Kuhusu ligi ni kweli kwamba ni ngumu, lakini kwa bahati nzuri hii sio mara yangu ya kwanza kucheza. Nina uzoefu wa kutosha tu, hivyo nipo tayari kuwa msaada kwa timu yangu.”

Wakati akiwa Saudia Arabia msimu uliopita, Msuva alipachika mabao manane na kuisaidia Al-Qadsiah kusalia kwenye Ligi Daraja la Kwanza nchini humo. Kuna kipindi timu hiyo ilikuwa kati ya nne ambazo zilikuwa kwenye hatari ya kushuka daraja.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YA SOKALEO, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here