KIMATAIFA
AL AHLY WASOTA GHANA, WAOMBA MECHI KUSONGEZWA MBELE
Mabingwa wa Afrika kwa ngazi ya klabu Al Ahly kutoka nchini Misri wamejikuta katika wakati mgumu wakiwa huko nchini Ghana baada ya kuwasili siku ya Jumatano tayari kwa mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mediama ya Ghana.
Taarifa iliyotolewa na timu hiyo imeeleza kuwa baada ya kuwasili Accra siku ya Jumatano walipata hitilafu ya ndege waliosafiria na juhudi za kutafuta usafiri wa kuwafikisha Mji wa Kumasi utakapochezwa mchezo wao zilishindikana kwa muda huo.
Kadhia hiyo imewafanya mabingwa hao wa kihistoria katika Ligi ya Mabingwa Afrika kuandika barua kunako Shirikisho la Mpira Afrika (CAF) na kuomba mchezo huo upigwe Jumamosi na si siku ya Ijumaa kama ilivyopangwa.