WAAMUZI WA MECHI YA SIMBA NA YANGA TAREHE 19.10.2024, UAMUZI SAHIHI UTUMIKE
Kesho Jumamosi mashabiki wa soka watashuhudia mchezo wa Kariakoo Dabi kati ya Simba dhidi ya Yanga ambao umekuwa ukisubiriwa kwa hamu kubwa kutokana na ushindani wa timu hizo.
Kariakoo Dabi haijawahi kuwa nyepesi hata siku moja ndiyo maana mchezo huo umekuwa kivutio kikubwa kwa watazamaji. Ukiangalia tayari Simba na Yanga zimekutana katika Ngao ya Jamii, Yanga imeshinda bao 1-0, kisha kutakuwa na mechi mbili za Ligi Kuu moja ikichezwa kesho.
Waamuzi ambao watapewa dhamana ya kusimamia sheria 17 za soka katika mchezo huu wana jukumu la kuifanya kazi yao kwa weledi mkubwa ili mambo yaende sawa. Imani yetu kubwa ni kwamba waamuzi wamekuwa wakitenda haki lakini hata pale wanapoteleza iwe kibinadamu na kusiwe na ishara ya kupendelea ambayo itakuja kuharibu kila kitu.
Jambo kubwa ni kwamba waamuzi ndiyo watu wa mwisho katika kutoa uamuzi ndani ya uwanja, hivyo katika kupewa dhamana hiyo itendeeni haki na si vinginevyo. Tulishuhudia dabi ya mwisho Yanga na Simba walipokutana kulikuwa na malalamiko ya waamuzi, tukio la Kelvin Kijili kuchezewa faulo ndani ya boksi.
Kariakoo Derby huwa inabeba mambo mengi, hivyo isitokee yeyote wa kufanya kitu cha kuharibu.Yote kwa yote, kila timu inasaka rekodi zake na mwendelezo mzuri ndani ya Ligi katika kuuwania ubingwa hivyo matokeo ya mchezo huu ni muhimu.