BAADA ya kijana mdogo kuonekanakutopata nafasi ya kucheza katika mitaa ya Jangwani, Denis Nkane kijana mdogo mwenye kipaji kikubwa huenda ndoto zake za kusaka kabumbu hadi ulaya zinaweza kutotimia.
Alipotoka Biashara Utd ya Mara kujiunga na Yanga, alikutana na kocha Nasradinne Nabi ambapo alikuwa akipata nafasi ya kuanza na kucheza, lakini tangu Nabi aondoke na ujio wa Miguel Gamondi umempa wakati mgumu Denis Nkane.
Mchambuzi wa michezo wa Wasafi Media Edo Kumwembe ametoa nasaha zake kwa kijana huyu, na kumlinganisha na Mrisho Ngassa Legend wa Yanga, aliyewahi kukipiga mitaa ya Msimbazi pale Simba.
“Denis Nkane anatabasamu na anacheka. Haoni tatizo la msingi linalomkabili. Huwa napenda kutazama picha zake wakati Yanga ikiwa kambini, au safarini. Anafurahia maisha ya Yanga vilivyo. Yanga wana maisha mazuri kwa sasa. Ndani na nje ya uwanja.
Wakati fulani Nkane alitajwa kuwa ‘Mrisho Ngassa mpya’ katika mpira wetu. Alionekana kama vile angeweza kufuata nyayo za Uncle Ngassa. Kwa kinachoendelea kwa sasa hakuna dalili kama anaweza kuwa Ngassa mpya katika mpira wetu.“
“Ngassa alikuwa anatabasamu, lakini alikuwa ana njaa moyoni mwake. Baadaye akalishika taifa. Akawa tegemeo la Yanga na timu ya taifa. Nkane ameridhika kabla hajawa Ngassa. Hatuioni hasira yake ndani ya uwanja wala nje ya uwanja.
“Ana msimu wa tatu pale Yanga, lakini hachezi. Hana nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza na hana nafasi ya kudumu hata katika wachezaji wanaokaa benchi. Achilia mbali kutoanza katika mechi, lakini Yanga inaweza kufanya mabadiliko ya wachezaji wa nne uwanjani na usitarajie kama Nkane ataingia.
“Nini kinatokea? Nkane anawakilisha tu tabia za wachezaji wetu wazawa. Hawana presha na maisha kama Watanzania wengi tulivyo. Nimeambiwa tu kwamba Nkane alikataa kuondoka kwa mkopo mwishoni mwa msimu wa uliopita. Anafurahia kuwa katika kundi kubwa la wachezaji wa Yanga. Alisema Edo Kumwembe.