UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa kuna ugumu kwenye kutengeneza nafasi za wazi katika mechi za ushindani jambo linalowafanya kutumia mbinu nyingine kusaka ushindi.
Kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara ubao wa Uwanja wa KMC, Mwenge ulisoma Simba 3-0 Tabora United mabao yakifungwa na Che Malone dakika ya 14, Valentino Mashaka dakika ya 64 na Awesu Awesu dakika ya 90.
Ni mchezo wa kwanza kwa Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids kwenye ushindani akiwa katika ardhi ya Tanzania kwenye Ligi Kuu Bara baada ya kutoka kambini Misri na timu hiyo itakayopeperusha bendera ya Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho.
Ahmed Ally Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa kuna ushindani mkubwa kwenye mechi ambazo wanacheza huku wachezaji wakijituma kupata nafasi za kufunga kwa kila mbinu.
“Katika mchezo wetu dhidi ya Tabora United uliochezwa Uwanja wa KMC unaona ilikuwa ngumu kutengeneza nafasi za wazi ndani ya 18 hivyo ilikuwa inatumika mipira inayotumwa kutoka mbali na wachezaji wetu na kupitia hiyo ikatupa matokeo na pointi tatu muhimu.
“Ukiangalia bao la Valentino ilikuwa pasi ndefu kutoka kwa Zimbwe hata bao la Awesu alikuwa ni Kibu Dennis alitoa pasi ambayo ilileta bao bado kuna maboresho yanakuja na furaha inakuja kwa Wanasimba.”