Mshambuliaji hatari wa Napoli na timu ya Taifa ya Nigeria, Victor Osimhen anadaiwa kuzikataa Chelsea na Arsenal na amepanga kusubiri hadi dakika ya mwisho ya dirisha hili la usajili ili kujiunga na Paris Saint-Germain.
Mshambuliaji huyo wa Napoli ana kipengele cha kuachiliwa ikiwa timu inayomhitaji itatoa Pauni 100 milioni.
Timu mbalimbali za England zimekuwa zikitaka kumsajili staa huyu mweny umri wa miaka 25 kwa miaka miwili sasa.
Hadi kufikia sasa Chelsea na Arsenal zote zinahitaji saini ya fundi huyu lakini Osimhen mwenyewe anaonekana kuwa na mpango wa kutaka kutua Ufaransa.
Hata hivyo, mwandishi wa habari kutoka Skysports, Florian Plettenberg amefichua kwamba PSG italazimika kuuza baadhi ya wachezaji kwanza kabla ya kufanikisha usajili wa staa huyo.
Miongoni mwa mastaa ambao PSG imepanga kuwauza kwa ajili ya kuipata huduma ya Osimhen ni Goncalo Ramos na Randal Kolo Muani.
Osimhen yupo tayari kusubiri hadi siku ya mwisho ya usajili kwani anaamini ataenda kupata nafasi kubwa ya kucheza na kuwika zaidi ikiwa ataenda PSG badala ya timu nyingine zinazomhitaji.
Staa huyu anadaiwa kuwaambia watu wake wa karibu kwamba iwe itakavyokuwa lazima ataondoka Napoli katika dirisha hili.
Mchezaji huyo wa zamani wa Lille anavutiwa sana na mpango wa kwenda kumrithi Kylian Mbappe na heshima ambayo anaweza kuipata akiwa na matajiri hao wa Jiji la Paris.