Ni safari ya zaidi ya miaka 30, ni safari ambayo wengi waliitamani, mapinduzi makubwa ya kisoka nchini yameanza kuja, uongozi mzuri wa vilabu ushindani wa vilabu nchini, makocha, wachezaji na hata uelewa kwa mashabiki pia ni sehemu ya mafanikio na hatua ambayo tunaendelea kupiga.
Wacha ni kurejeshe nyuma kidogo miaka 15 iliyopita, vita ilikuwa ni ya Simba na Yanga SC tu siyo kwenye msimamo wa Ligi wala kwenye kupata wachezaji bila hata kusahau kuajiri makocha kutoka nje na kisajili wachezaji bora wa kigeni.
Muda huo ulikuwa muda wao wa kutamba kwenye kila idara kusikia majina ya makocha kutoka Serbia, Uholanzi, Belgium, Brazil, Ufaransa basi ni dhahiri shahiri jibu la haraka na sahihi ni kuwa asipokuwa kocha wa Simba SC basi ni upande wa Pili Yanga SC, hakukuwa na nafasi nyingine kwa vilabu vingine kuonekana kuwa vinaweza kushindana na vigogo hao nchini.
Ila kwa sasa kila kitu kimebadilika nchini, sasa kila timu inataka kufanya vizuri kuanzia ndani ya uwanja mpaka nje ya uwanja. Vilabu vingi vilikuwa vikitumia wachezaji wazawa kwa kiasi kikubwa pamoja na makocha wazawa pia, ila sasa ni tofauti pia. Siyo ajabu kusikia klabu iliyopanda daraja imeajiri kocha mgeni na zaidi ya wachezaji watano wa nje.
Licha ya hivyo vilabu vyote 16 vina wachezaji wa kigeni siyo masihara ila ni dhahiri kuwa vilabu vingi vinatamani sana kufanikiwa kufanya vizuri na kuonyesha upinzani mkubwa kwenye Ligi yetu.
Nje ya ilo ni ushiriki wetu wa kimataifa miaka mingi tumeona asiposhiriki Simba SC basi ni Yanga SC tu na ilo halina ubishi kuwa wameongeza thamani ya Ligi yetu na kwa sasa tuna nafasi ya kuwakilisha timu nne kimataifa kwa kila msimu. Jambo zuri na kubwa ni kuwa kila msimu lazima timu moja tofauti ya vigogo nchini Yanga SC, Simba SC na Azam FC akishiriki kimataifa.
Tulianza kumuona Namungo FC, Biashara United, KMC FC na Mtibwa Sugar wakishiriki michuano hiyo na sasa Coastal Union, ni muda ambao sasa nje ya vilabu hivyo vikubwa tunashuhudia vilabu vingine navyo vikipata nafasi ya kushiriki kwa nyakati tofauti tafauti.
Upande wa uongozi vilabu vimebadilika sasa nafasi nyingi wanapewa watu wa kimpira zaidi kuliko hapo nyuma ni ngumu sasa kusikia kamati nyingi na kila mara zikitangazwa ndani ya vilabu vyetu jambo ambalo linatupa mwanga wa mabadiliko hayo mfano halisi ni Thabiti Kandoro pale Kagera Sugar.
Udhamini sasa ndiyo eneo pekee ambalo hakuna haja ya kuongea sana linaonekana vilabu vingi sasa robo tatu yao wana udhamini jezi zimejaa wadhamini wakutosha toa Azam FC, Yanga SC na Simba SC ambao mara zote wamekuwa na wadhamini alafu njoo tugeukie upande mwingine Singida Blacks Stars ina zaidi ya wadhamini wanne, Coastal Union pia, siyo hao tu Pamba Jiji, Namungo FC, Mashujaa FC je.
Hiyo ni njia tosha kuona mapinduzi makubwa yakifanyika kwa sasa ni ngumu kusikia timu imekwama kusafiri kwa sababu ya hela, malalamiko ya mishahara imepungua kwa kiwango kikubwa sana ni nadra kusikia mchezaji hajalipwa mshahara wake jambo ambalo hapo nyuma kelele hizo zilikuwa nyingi sana, kwa kifupi wacha tujipongeze kwa hatua hii ambayo tumepiga sasa.
Kama nimesahau wacha nikukumbushe kuwa MVP wengi sasa wanakuja nchini kwetu Wafungaji bora wa Ligi nyingine nao wanatamani kusakata kabumbu ndani ya ardhi hii ya Tanzania, wacha nimalizie kwa kuwakumbusha kuwa kwa sasa tuna Ligi za vijana kuanzia U-15, U-17 na U-20 pia taifa tuna maeneo mawili makubwa na rasmi kwa ajili ya kambi na sehemu ya kuchezea kwa vijana wadogo ambavyo vinapatikana Tanga, na Kigamboni, Dar es Salaam.