Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, aliuzungumzia usajili wa Leonel Ateba ulivyokuwa, huku akisema walikuwa na machaguo mengi lakini kura ya ‘ndio’ ikamwangukia Ateba.
“Tumemsajili Ateba kutokana na kiwango alichonacho, hatukumtoa nyumbani, tumemtoa kwenye timu yake ya USM Alger na alikuwa tayari amefanya mazoezi ya utimamu wa mwili na kikosi chake, alikuwa anataka kujiandaa na majukumu mapya, sisi tukamchomoa, tumemnunua kwa fedha nyingi na hatimaye ametua kwa mkataba wa miaka miwili.
Mimi nina imani naye na mashabiki wa Simba SC nadhani nao wana imani naye, na niwaambie tu, moja kwa moja anaingia kwenye kikosi, hahitaji mazoezi ya peke yake, hata kesho (leo), anaweza kupewa jezi na akacheza,” alisema Ahmed.
Akiwa kwao Cameroon, alifunga mabao 40 katika michezo 48, kabla ya kuhamia Algeria kwenye klabu yake mpya, ambako amefunga magoli matatu na kutoa ‘asisti’ 11.
Nyota huyo anapishana na Willy Onana, ambaye Simba imemuuza kwa klabu ya Al Hilal Benghazi ya Libya baada ya kukubali dau walilowatajia.