KITAIFA

AZIZ KI ATOBOA UKARIBU WAKE NA CHAMA ULIPOANZIA

MFUNGAJI Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, aziz ki, amefichua siri baina yake na mchezaji mpya kwenye klabu hiyo, Clatous Chama kuwa kila mmoja alitaka kucheza timu moja na mwenzake.

Aziz Ki, ambaye msimu uliopita alikuwa mchezaji tegemeo kwenye kikosi hicho, akiibuka pia mfungaji bora wa Ligi Kuu kwa kupachika mabao 21, amesema kwa muda sasa kila mmoja alikuwa akimpongeza mwenzake anapofanya vema katika michezo mbalimbali na kutamani siku moja wakutane kwenye timu moja.

“Chama ni mchezaji mzuri sana, tangu yupo Simba alikuwa akinikubali, akinipa pongezi mara kwa mara na kusema anataka kucheza timu moja na mimi, hata mimi mwenyewe kutokana na kuona jinsi alivyokuwa akifanya akiwa na kikosi chake nilitamani pia siku moja kucheza naye na ndoto hii hatimaye imetimia, tuko wote Yanga,” alisema Aziz Ki.

Kuhusu ufungaji bora msimu ujao, kiungo mshambuliaji huyo anayechezea pia timu ya taifa ya Burkina Faso, ametabiri kiatu cha dhahabu msimu ujao kitabaki Yanga, akiwataja wachezaji Kennedy Musonda, Clement Mzize au Prince Dube mmoja wao ni lazima akivae.

“Nadhani msimu huu tutakwenda mbali zaidi kwa sababu tumesajili wachezaji wazuri sana, nina imani kikosi chetu kitakuwa tishio zaidi.

“Kikosi bado kina Pacome, Maxi na sasa kimeongezewa uwezo wa Chama na Prince Dube, kusema kweli kiko imara na tunaweza kufanya makubwa zaidi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, nadhani hata ufungaji bora msimu ujao utabaki kwetu, tuna Mzize, Musonda, halafu kuna Dube, yaani msimu ujao mfungaji bora atatokea tena Yanga,” alisema.

Mchezaji huyo ambaye usajili wake kuelekea msimu ujao ulizua gumzo kubwa kwenye vyombo vya habari kutokana na kuonekana kutakiwa na klabu kadhaa za Afrika, alisema ana uhakika mashabiki wa Yanga watasafiri kwa wingi kueleka Burundi kama mechi yao ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika itachezwa huko.

“Nina imani mashabiki wengi watajitokeza kwenda Burundi ili kutupa sapoti kwa sababu niliona msimu uliopita walivyojitokeza kwa wingi kwenda Rwanda katika mechi yetu dhidi ya Al Merrikh, timu hii ina mashabiki ambao ni kama familia moja, wako karibu sana na timu yao.”

Msimu uliopita mashabiki wengi wa Yanga walisafiri mpaka Rwanda katika mechi yao ya raundi ya kwanza dhidi ya timu hiyo ya Sudan ambapo kwa kiasi kikubwa iliwasaidia kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, Septemba 16 mwaka 2023 na kuweza kutinga hatua ya makundi.

El Merrikh ilishindwa kucheza kwenye ardhi yao kutokana na machafuko ya kisiasa.

Hata hivyo zipo habari kuwa Vital’O huenda isitumie uwanja wa nyumbani kwao kutokana na kutokidhi vigezo vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button