TUMEPOKEA MAOMBI YA SIMBA KUSAFIRISHA MASHABIKI WAO KWENDA MISRI

Naibu Waziri wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma amesema kuwa Serikali imepokea maombi ya Klabu ya Simba ya kupeleka mashabiki wake Misri kwa ajili ya kuiunga mkono timu hiyo kwenye mchezo wa mkondo wa pili wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly.
“Tulianza kupokea maombi ya klabu ya Yanga kuwasafirisha mashabiki na jana tumewaaga, baada ya hilo klabu ya Simba nayo ikatutumia maombi, tumeyapokea na tunayashughulikia na naamini mashabiki wa klabu ya simba nao watapata nafasi ya kwenda kuishabikia timu yao”
Mwinjuma ameyasema hayo nje ya Ukumbi wa Bunge leo Jumanne, Aprili 2, 2024 mara baada kikao cha kwanza cha mkutano wa 15 wa Bunge la 12 unaoendelea jijini Dodoma.
Aidha kuhusu mapokezi ya timu hiyo, Mwinjuma amesema balozi za Tanzania kwenye nchi za Afrika ya Kusini na Misri zinafanya kazi kwa karibu na klabu hizo ili kuhakikisha hakuna jambo litakaloleta changamoto.