ALIYEKUWA nyota wa TP Mazembe na timu ya taifa ya Zambia, Rainfold Kalaba amerejewa na fahamu na sasa anaweza kuzungumza na kula.
Akitoa taarifa hiyo leo Ijumaa, Ofisa Uhusiano wa University Teaching Hospital (UTH), Nzeba Chanda, amesema kwamba Kalaba baada ya kupata nafuu amefanikiwa kupata mlo wa kwanza tangu ajali hiyo ilipotokea Jumamosi iliyopita.
“Hali ya Kalaba imeimarika sana. Leo alipata mlo wake wa kwanza, yuko na fahamu kabisa na anaweza kuzungumza,” amesema ofisa huyo.
“Bado timu ya matibabu inaendelea kumuangalia kwa ukaribu zaidi maendeleo ya afya yake. Tutaendelea kuwajulisha wananchi kwa ujumla kuhusu hali yake.”
Kalaba alipata ajali katika Barabara ya Great North eneo la Kafue huko Zambia, baada ya gari aliyokuwemo kugongana na roli la mafuta.