Kiungo wa Yanga SC, Stephanie Aziz Ki, amesema ana furahi kuona ile ahadi yake ya kufunga bao katika Kariakoo Dabi, ameitimiza.
Aziz Ki alimuahidi Mjumbe wa Baraza la Wadhamini la Yanga, Antony Mavunde ambaye pia ni Waziri wa Madini na Mbunge wa Dodoma Mjini, kwamba atafunga bao kwa ajili yake na kweli amefanya hivyo baada ya kufunga bao la kwanza kwa penalti, kabla ya Joseph Guede kuongeza la pili wakati Yanga ikishinda 2-1. Lile la Simba lilifungwa na Freddy Michael.
“Haikuwa rahisi, ninajisikia furaha na ninasikia fahari kwa Wananchi, viongozi wote wa Yanga na wachezaji kwa sababu dabi ni dabi, lazima ushinde.
“Kabla ya dabi nilimuahidi Mavunde nitafunga kwa ajili yake leo, nikamuita aje uwanjani kwani nataka kufunga mbele yake, kwa hiyo leo nina furaha kubwa kwa sababu nimesema kitu na kufanya kweli,” amesema Aziz Ki ambaye amefikisha mabao 15 katika Ligi Kuu msimu huu.
Akizungumzia ahadi aliyopewa na kutimizwa, Mavunde amesema: “Kwanza ile penalti sikuiangalia, niligeukia upande wa pili kwa sababu nilijua kwamba kile alichoniahidi anakwenda kukitimiza, kwa hiyo nilikuwa na furaha kubwa sana kwa sababu ni kweli leo aliniambia atafunga kwa ajili yangu, ni rafiki yangu sana.
“Kwa hiyo nimefurahi sana, wakati inafungwa ile penalti nilikuwa na furaha kubwa sana kwa sababu ya rafiki yangu.”
Kuhusu ubingwa, Mavunde amesema: “Kama kulikuwa na kizuizi kikubwa ilikuwa leo, naamini kabisa kwa mechi zilizobaki ingawa ligi ni ngumu, nafasi ya ni kubwa sana ya kuchukua ubingwa.”
Yanga imefikisha pointi 58 baada ya kucheza mechi 22, imebakiwa na michezo nane kukamilisha msimu huu ambapo inatakiwa kushinda mechi sita ili kufikisha pointi 76 na kutetea ubingwa kwani hazitafikiwa na wapinzani wake wa karibuni, Azam (51) na Simba (46).