Msikiti wa Samatta

Ule msikiti uliojengwa na nyota wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga klabu ya PAOK ya Ugiriki, Mbwana Samatta umezinduliwa rasmi juzi Ijumaa ukiwa na uwezo wa kuingia waumini 5,000 kwa wakati mmoja.

Msikiti huo uliopewa jina la Masjid Samatta, upo Vikindu wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani, ambako baba wa staa huyo, Ally Samatta Pazi aliukabidhi rasmi kwa wakazi wa eneo hilo.

Mzee Samatta amesema, ana furaha kubwa kuona kijana wake amerudisha shukrani kwa Mungu na jamii, anaamini kupitia hilo ataendelea kupata baraka kwenye jukumu lake kama mwanasoka.

“Ni jambo jema kumkumbuka Muumba kwenye ujana wake, pamoja na neema anazozipata maishani mwake bila Mungu ni bure, ndio maana akiniambia anataka kufanya vitu vya huduma kwa wengine na kuwa mstari wa mbele kuvisapoti,” amesema Mzee Samatta na kuongeza;

“Baada ya kumaliza shughuli za uzinduzi, akapigiwa simu, jambo alilosema anajisikia faraja kuona watu wanapata sehemu nzuri ya kuabudia, akawashukuru mashekhe waliojitokeza jana na akawatakia kazi njema katika utumiahi wao.”

“Samatta sio muongeaji, lakini anajitoa sana kwa jamii bila kubagua, hilo linanigusa kama mzazi, kuna wengine nimewasikia wakisema sasa angekujengea ghorofa, nawaambia ninalo la kwangu nililojenga kwenye ujana wangu, hivyo anachokifanya ni bora zaidi,” amesema Mzee Samatta ambaye enzi za ujana wake naye alikuwa mahiri katika soka kama ilivyo kwa mwanae aliyeanza kuwika akiwa na Mbagala Market, Simba kisha kwenda DR Congo kuichezea TP Mazembe na kuuzwa KRC Genk ya Ubelgiji na kupita pia timu za Aston Villa inayoshiriki Ligi Kuu ya England (EPL).

Msikiti huo wa Samatta ulianza kujengwa mwaka 2018 na  Mzee Samatta amesema ameona kama ametua mzigo kwa kuzinduliwa na kuanza kutumia na roho yake ina amani kubwa.

Hata hivyo, thamani halisi wa msikiti huo hajaiwekwa wazi kutokana na nyota huyo wa timu ya taifa, Taifa Stars kuwa msiri katika mambo yake mengi.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YA SOKALEO, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here