Asec Mimosas simba, simba shirikisho caf

SIMBA watakuwa ugenini kuwavaa Asec Mimosas Ijumaa katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika huku wakikosa huduma ya kipa Ayoub Lakred na winga Willy Onana, lakini unaambiwa wala hawana presha.

Iko hivi; Onana na Ayoub wameachwa Dar es Salaam kwa sababu mbalimbali, lakini kipa ana kadi tatu za njano ambazo kwa mujibu wa kanuni za CAF anatakiwa kukosa mchezo mmoja huku Onana akisumbuliwa na nyama za paja.

Wawili hao kukosekana kwao wala hakuwapi shida Simba kwa mujibu wa kocha wa makipa wa timu hiyo, Daniel Cadena aliyesema hawana wasiwasi kwa sababu eneo la kipa limesheheni vipaji vikubwa na vyenye uzoefu.

“Simba ipo vizuri hasa kwenye eneo la makipa. Tuna wachezaji wengi wazuri na wazoefu. Aishi Manula ni kipa ambaye ametoka kucheza michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) na ana uzoefu wa michuano ya kimataifa akiisaidia Simba kufika hatua ya robo fainali kimataifa katika misimu mitatu nyuma,” amesema Cadena.

“Ukija kwa upande wa Ally Salum pia ni kipa ambaye anaaminiwa na amefanya kazi kubwa kwenye michuano ya kimataifa msimu uliopita. Aishi akiwa nje ya uwanja kwa majeraha (Salim) ameonyesha uwezo mkubwa, hivyo ana uzoefu.”

Cadena amesema katika eneo hilo hawana wasiwasi wowote wakiwa wanaamini waliopo watafanya vizuri na timu kuweza kufikia malengo, huku akimzungumzia kipa Hussein Abel kuwa yeye pia ni mzuri.

“Abel ni kipa mzuri, lakini amekutana na makipa wazoefu na ndio maana anakosa namba, ila naamini akiaminiwa na kupewa nafasi anaweza kufanya vizuri. Mimi kama kocha nitaendelea kumfua na kumjengea kujiamini,” amesema.

Wakati Cadena akifunguka hayo, Hizi hapa data za Ayoub na Onana kwenye mechi kimataifa a mechi tano za Ligi Kuu Bara za hivi karibuni.

Onana licha ya kukosa mechi tano za ligi mara baada ya kusimama kupisha Afcon, ndiye aliyerejesha matumaini ya Simba baada ya kuifungia timu hiyo mabao 2-0 dhidi ya Wydad katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Naye Ayoub licha ya kufanya vizuri kwenye mechi za ligi za hivi karibuni, pia amecheza dakika zote kwenye mechi za kimataifa akiisaidia timu hiyo kwenye baadhi ya mechi ikiwamo dhidi ya Jwaneng Galaxy ambayo Wekundu wa Msimbazi waliambulia sare.

Simba ipo katika nafasi ya pili kwenye kundi B la Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kucheza mechi nne ikikusanya pointi tano imeshinda moja, sare mbili na kufungwa moja.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YA SOKALEO, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here