MSHAMBULIAJI wa Yanga, Jean Baleke ameweka wazi kuwa bado kazi ipo kwenye ligi na atacheza mechi nyingi kwa kuwa ligi inaanza na benchi la ufundi lina hesabu zake.
Ipo wazi kwamba Balake ni ingizo jipya ndani ya Yanga aliwahi kucheza kikosi cha Simba msimu wa 2023/24 na alifunga jumla ya mabao 8 kabla kukutana na Thank You kutoka kwa mabosi wake wa zamani.
Oktoba 19 2024 ndani ya ligi inayodhaminiwa na NBC, Kariakoo Dabi inatarajiwa kuchezwa kwa mchezo wa ligi kati ya Simba dhidi ya Yanga Uwanja wa Mkapa ikiwa ni mzunguko wa kwanza kwa watani hao wa jadi kukutana uwanjani.
Baleke amesema mashabiki wamekuwa na maswali mengi kuhusu yeye kuanza kikosi cha kwanza jambo ambalo litajibiwa kwenye mechi ambazo zinafuata anaamini atacheza.
“Unaona kuna maswali mengi ambayo yanahusu mimi kucheza, angalia kwa sasa ligi inaanza na kuna mechi nyingi ambazo zipo kwa wakati huu nina amini kwamba nitacheza mechi nyingi na itakuwa hivyo kutokana na uwezo ambao ninao.
“Kila mchezaji anauwezo mkubwa ndani ya timu hilo lipo wazi hivyo benchi la ufundi linafanyia kazi makosa ambayo yanatokea kwenye mechi zilizopita ili kuwa bora zaidi na tunaamini tutakuwa imara.”
Kwenye mchezo dhidi ya Pamba Jiji uliochezwa Uwanja wa Azam Complex wakati ubao ukisoma Yanga 4-0 Pamba Jiji alisababisha penalti moja dakika ya 44 ikafungwa na Aziz Ki dakika ya 45.