MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara Yanga chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi wamebainisha kuwa mpango mkubwa ni kupata matokeo kwenye mchezo wao wa ligi dhidi ya Kagera Sugar.
Huo utakuwa ni mchezo wa kwanza kwa Yanga inayonolewa na Gamondi ambaye alikuwa katika kikosi msimu wa 2023/24 na kushuhudia timu ikigotea nafasi ya kwanza na pointi 80 kibindoni.
Agosti 29 2024 itakuwa Uwanja wa Kaitaba, kusaka pointi tatu dhidi ya Kagera Sugar ambao nao wanazihitaji pointi hizo baada ya kupoteza mchezo wao uliopita dhidi ya Singida Black Stars walipofungwa bao 1-0 Uwanja wa Kaitaba.
Dickson Job beki wa Yanga ameweka wazi kuwa wapo tayari kwa msimu mpya na kikubwa ni sapoti kutoka kwa mashabiki wao ambao wamekuwa nao bega kwa bega.
“Tupo tayari kuelekea mchezo wetu dhidi ya Kagera Sugar na mwanzo wa msimu tunahitaji kuanza vizuri hivyo mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi na waendelee kuwa bega kwa bega nasi tuna amini tutafanya vizuri.’
Vinara wa ligi kwa sasa ni Simba baada ya mechi mbili wamevuna pointi sita huku safu ya ushambuliaji ikifunga jumla ya mabao 7.