SHIRIKISHO la Soka Tanzania, (TFF) limetoa taarifa kuwa Yanga imefungiwa kufanya usajili kwa kukiuka kanuni za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu, (FIFA).
Taarifa hiyo imeeleza kuwa uamuzi huo umefanywa na FIFA baada ya timu hiyo kukiuka Annexe 3 ya kanuni ya Uhamisho wa Wachezaji, (RSTP) ya Shirikisho hilo.
Pamoja na masuala mengine Yanga haikuingiza uthibitisho wa malipo ya mchezaji husika katika Mfumo wa Usajili, (TMS) licha ya kukumbushwa kufanya hivyo.
Klabu hiyo imetakiwa kutekeleza matakwa ya kikanuni na kuwasilisha taarifa kwa Sekretarieti ya Kamati ya Nidhamu ya FIFA ambapo suala hilo limefikishwa kwa ajili ya hatua zaidi.
Taarifa ya TFF iliyotolewa Aprili 12 2024 kupitia kwa Ofisa Habari Cliford Ndimbo imeeleza kuwa kutokana na uamuzi huo wa FIFA, TFF imefungia Klabu ya Yanga kufanya usajili wa wachezaji wa ndani.