KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema watakuwa makini katika mchezo wao wa hatua ya 16 bora ya kombe la CRBD Bank Federation dhidi ya Dodoma Jiji FC, kwani ni timu iliyowasumbua kwenye mechi ya Ligi Kuu, huku akihofia wachezaji wake kubweteka baada ya kutoka kucheza michuano mikubwa ya Ligi ya Mabiongwa Afrika.
Kikosi cha Yanga kimeondoka kuelekea Dodoma kwa ajili ya mchezo huo utakaochezwa kesho (Jumatano), kwenye dimba la Jamhuri, jijini humo.
Gamondi amesema wamejipanga vizuri kulingana na mchezo huo kuwa mgumu kwa sababu mashindano hayo ni mtoano na anapofungwa anatoka.
Amesema walipata muda mfupi wa kufanya mazoezi kwa sababu ya kutoka katika mashindano makubwa na anaimani Dodoma Jiji FC, mara ya mwisho iliwasumbua.
“Hautakuwa mechi rahisi kwa sababu Dodoma Jiji FC ni wazuri na tuliwahi kucheza nao nyumbani na walitusumbua, mchezo huu tunatakiwa kuwa makini na kucheza kwa tahadhari kubwa ili kufuzu kucheza robo fainali,” amesema Gamondi.
Ameongeza kuwa wanahitaji kutetea mataji yao, kufanikiwa katika malengo yao ni kushinda mchezo wao dhidi ya Dodoma Jiji FC ili kucheza robo fainali na baadae fainali.
Gamondi amesema licha ya kuwakosa baadhi ya wachezaji kutokana na sababu mbalimbalu lakini anaimani na wachezaji wake kupambana na kupata matokeo mazuri mbele ya wapinzani wao hao.