UONGOZI wa Simba umebainisha kuwa matokeo ambayo wanayapata yanaumiza kwelikweli kwa kuwa ni mabaya ndani ya muda mfupi.
Ipo wazi kwamba Aprili 6 2024 kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali baada ya dakika 90 ubao ulisoma Al Ahly 2-0 Simba.
Kwenye mechi mbili za kimataifa Simba imefungwa mabao matatu huku safu yao ya ushambuliaji ikikwama kufunga hata bao kwa wapinzani wao.
Wakarejea tena Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma ubao ukasoma Mashujaa 1-1 Simba walipofika katika changamoto ya penalti ilikuwa Mashujaa 6-5 Simba ilikuwa ni Aprili 9 2024.
Ndani ya siku tatu Simba imefungashiwa virago katika mashindano mawili makubwa, Ligi ya Mabingwa Afrika na CRDB Federation Cup.
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema: “Inaumiza kwa kweli matokeo ambayo tunayapata. Kupata matokeo mabaya ndani ya siku tatu inaumiza kwelikweli,”.
Kituo kinachofuata ni Aprili 13 dhidi ya Ihefu, Uwanja wa Liti ambapo Simba itakuwa ugenini.