RAIS wa CAF, Patrice Motsepe, 61, ni tajiri mkubwa sana. Kiufupi anaogelea kwenye bahari ya pesa.
Yeye ni mfanyabiashara mkubwa, bilionea wa madini wa Afrika Kusini, ambaye pia ni mmiliki wa klabu ya Mamelodi Sundwons. Anashika namba 1,307 katika orodha ya watu matajiri zaidi duniani kwa mujibu wa Jarida la Forbes, akimiliki utajiri wenye thamani ya Dola 3.1 bilioni.
Patrice Motsepe alizaliwa kwa baba Kgosi Augustine Motsepe, chifu wa Wammakau ambao ni tawi la watu wa jamii ya Watswana. Mzazi wake awali alikuwa mwalimu wa shule na baadaye akawa mfanyabiashara mdogo anayemiliki kioski ambacho kilikuwa maarufu sana kwa wafanyakazi wa migodini. Ilikuwa ni kutokea katika duka hili dogo ambako Motsepe alijifunza misingi ya biashara kutoka kwa baba yake, pamoja na kuanza kuijua biashara ya madini.
Akapata digrii ya sanaa katika Chuo Kikuu cha Swaziland na kisha digrii ya sheria katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand. Akabobea katika madini na sheria.
Huyu ndiye mwamba Motsepe kwa kumuelezea kwa ufupi. Ni bilionea, ni msomi. Na Rais wa Shirikisho la Soka la Afrika (Caf).
Tangu ameingia madarakani ameonekana ni Rais mwenye kutaka kuona soka la Afrika linafanikiwa na anaamini kila jambo linawezekana akijiangalia yeye alikotokea katika maisha ya chini hadi kuwa bilionea mkubwa Afrika na duniani.
Lakini katika mambo yanayoweza kutia doa utawala wake ni ligi ya majaribio ya African Football League (AFL), ambayo ilikataliwa Ulaya, ikaletwa na kina Gianni Infantino, Rais wa Fifa, ijaribiwe Afrika.
African Football League ndio ileile Super League iliyoanzishwa na kina Florentino Perez wa Real Madrid na wenzake wa Barcelona na kupingwa vikali na mashabiki na magwiji wa soka wa England hadi kufikia baadhi ya vyama vya soka kutishia kuzikata pointi 15 timu ambazo zingejumuika kushiriki ligi hiyo ya pesa.
Baada ya upinzani mkubwa kutoka kwa mashabiki wa England, mpango wa kuanzishwa kwa European Super League ulionekana kama umekufa. Lakini kumbe wala haujafa. Florentino Perez hakuweka silaha chini kwa sababu bado anaamini soka ni mchezo wa maokoto na klabu zitatajirika sana kama zitafanikisha ligi hiyo ya pesa.
Marufuku zilizopigwa hazikumtisha Perez na watu wake. Wakatinga mahakamani na kuibuka wababe baada ya Mahakama Kuu ya Ulaya (European Court of Justice) kutoa hukumu kwamba UEFA na FIFA zimevunja sheria ya haki ya ushindani kwa kutishia kuziadhibu klabu zitakazojiunga na mpango wa kushiriki Super League.
Hukumu hiyo ikawapa uhuru waandaji wa Super League ambao wamekuja na mpango mpya wa kuandaa ligi itakayoshirikisha timu 64 na huku pia wakitaka michuano yao hiyo mipya ije kushindana na hata kuizika kabisa michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Europa League na Europa Conference League.
Baada ya taarifa hiyo ya waandaaji, timu nyingi Ulaya ambazo awali zilionyesha nia ya kushiriki michuano hiyo, zikatoa taarifa za kujiweka kando nayo, ambayo wengine wanaamini ni jambo lililotokana na woga baada ya kutishiwa adhabu.
Na baada ya kuona timu zinazosapoti zimebaki chache, Rais wa UEFA, Aleksander Ceferin aliamua kurusha dongo akisema: “Natumai michuano hii itaanza haraka iwezekanvyo… ikiwa na timu mbili.”
Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Abidjan, Ivory Coast kunakofanyika fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka huu, Motsepe alisema uamuzi kutaka kuifuta michuano ya Kombe la Shirikisho unalenga kuyapa nguvu mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Ligi ya Afrika (AFL) ambayo yana manufaa makubwa zaidi kwa klabu.
Motsepe alisema kuwa gharama za uendeshaji na usimamizi wa mpira wa miguu ni kubwa hivyo ni vyema kubaki na mashindano machache yenye ufanisi na faida hivyo Caf inajiandaa kufuta Kombe la Shirikisho Afrika.
“Nahitaji kupata fedha kwa ajili ya nchi wanachama, tunahitaji fedha kwa ajili ya maendeleo na kuongeza zawadi kwa washindi katika mashindano. Al Ahly, Wydad na klabu kwenye Ligi ya Mabingwa hazipati fedha, zinapoteza fedha.
“Hivyo tunataka Ligi ya Mabingwa Afrika na AFL kuwa na nguvu kubwa ya kiuchumi na kufanya klabu zitengeneze fedha lakini kitu kingine cha msingi ni tunaweza kufuta Kombe la Shirikisho. Hatuwezi kuwa na mashindano mengi,” alisema Motsepe.
Ikiwa litafutwa, Kombe la Shirikisho Afrika litakuwa limedumu kwa muda wa miaka 21 tu kwani lilianza kwa mara ya kwanza mwaka 2003 baada ya kuunganishwa kwa mashindano ya Kombe la Caf na Kombe la washindi Afrika.
Kumbukumbu nzuri kwa timu ya Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika ni msimu uliopita ambapo Yanga ilitinga hatua ya fainali ambayo ilishindwa kutwaa ubingwa licha ya kutoka sare ya mabao 2-2 na USM Alger ya Algeria, ikiangushwa kwa sheria ya mabao mengi ya ugenini.
Wasiwasi wa mashabiki wa Ulaya, ndio huohuo wanaopaswa kuwa nao mashabiki wa Afrika kuhusu michuano AFL. Kuua michuano rasmi ya soka Afrika kwa ajili ya kujaribu kuinua michuano mipya ambayo itazinyima fursa timu ndogo kama Biashara United na Namungo kuonja michuano ya kimataifa, halipaswi kuwa jambo la kujivunia.
Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) linachezwa kuanzia ngazi ya chini kabisa kuanzia Ligi ya Mabingwa wa Mkoa hadi Ligi Kuu timu zikisaka ubingwa ili kupata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika. Timu nyingi sana zinashiriki katika mchakato huu.
Ligi ya AFL, kama inavyopangwa kuwa ligi ya pesa, inatarajiwa kuzishirikisha timu chache za Simba, Yanga na pengine na Azam (yaani zile zile ambazo utazikuta pia katika Ligi ya Mabingwa Afrika). Na kama ambavyo imezoeleka kwa timu hizo kuwa na nguvu ya kifedha, ushiriki wao kwenye AFL utaziongezea uwezo wa kifedha na kuzidi kuziacha timu za levo ya Mtibwa Sugar umbali wa sawa na mbingu na ardhi! Kwa Tanzania, tukifuta Kombe la ASFC, tutabaki na Ligi Kuu Bara tu na ligi za chini. Labda na Kombe la Mapinduzi. Ingawa Kombe la ASFC linaweza kubaki kuwa kama Kombe la Carabao la England ambalo bingwa haendi kokote, lakini kwa hakika mfumo wa sasa ambao bingwa anaenda kucheza michuano ya Afrika una mantiki zaidi.
Tayari kuna tofauti kubwa kati ya timu za juu kama Simba na Yanga na timu nyingine na kwa ushiriki wa AFL, tofauti hiyo itakuwa mara dufu.
SIKIA MAONI
Straika wa zamani wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’, anaona kwamba hatua ya Motsepe kuinua michuano ya AFL na kufuta Kombe la Shirikisho Afrika itazisaidia klabu kuinuka kiuchumi kwa kufanya mashindano yenye maana zaidi.
“Kwa mfano sasa hivi, baadhi ya timu zinafuzu Kombe la Shirikisho halafu zinashindwa kusafiri kwenda kwenye mechi zao, hii inafanya mashindano haya Kombe la Shirikisho kukosa maana,” alisema nyota huyo anayeshikilia rekodi ya muda wote ya kufunga mabao mengi katika msimu mmoja wa Ligi Kuu Bara ambapo alifungia Yanga mabao 26 mwaka 1999, rekodi ambayo imedumu kwa miaka 25 sasa.