ALIYEKUWA mshambuliaji wa Simba Mzambia, Moses Phiri amejiunga na Power Dynamos FC ya Zambia kwa mkataba wa miaka miwili.
Mshambuliaji huyo alikuwa akiichezea timu hiyo aliyojiunga nayo kwa mkopo Januari 16, mwaka huu akitokea Simba, baada ya kutokuwa na nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza hivyo kuamua kutafuta changamoto sehemu nyingine.
Phiri aliyejiunga na Simba Juni 15, 2022 amemaliza mkataba wa miaka miwili aliosaini na timu hiyo wakati anajiunga nayo akitokea Zanaco, japokuwa kulikuwa na kipengele cha kuongeza mwingine wa mwaka mmoja.
Akizungumza kutoka Zambia, Phiri amesema amekuwa na mazungumzo na baadhi ya timu, hivyo ataweka wazi hivi karibuni atakapokwenda kwa ajili ya msimu ujao, huku akiwataka mashabiki kuendelea kumpa sapoti.
“Timu nyingi zimeonyesha nia ya kuhitaji saini yangu, lakini bado sijafanya uamuzi wa mwisho wa wapi nitacheza msimu ujao. Suala hilo kwa sasa nimewaachia wawakilishi wangu walifanyie kazi na litakapokamilika nitaliongelea,” amesema.
Wakati akizungumza hayo, mmoja wa marafiki wa karibu wa mchezaji huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake ameliambia Mwanaspoti kwamba Phiri ameshasaini mkataba wa kuichezea Power Dynamos na tayari ameanza maandalizi ya msimu na kikosi hicho.
“Dynamos imetoka hapa makao makuu yake mjini Kitwe na imeenda mji mkuu wa Zambia (Lusaka) hapa hapa Zambia kwa ajili ya kuweka kambi ya maandalizi ya msimu, huku Phiri akiwa ni miongoni mwa nyota wapya waliosajiliwa,” amesema rafiki huyo.
Katika msimu wa kwanza kwa Phiri akiwa Simba ulikuwa bora kwani alifunga mabao 10 Ligi Kuu Bara nyuma ya vinara mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele na Said Ntibazonkiza ‘Saido’ wa Simba waliofunga mabao 17 kila mmoja.
Kwenye msimu uliopita hadi anaondoka nchini Januari, mwaka huu kurudi Zambia, nyota huyo alikuwa na mabao matatu Ligi Kuu Bara.
Wakati anajiunga Simba Juni 15, 2022, Phiri alitokea kushika nafasi ya pili akifunga mabao mengi katika Ligi Kuu Zambia akiwa na Zanaco alikofunga 14, nyuma ya mshambuliaji kinara na mfungaji bora, Ricky Banda wa Red Arrows aliyefunga 16.