Chama kuondoka simba

UONGOZI wa SIMBA unatajwa kumpatia masharti mazito mchazeji wao Clatous Chama ambaye mkataba wake na miamba hiyo umeisha, ili wakamilishe kumpatia mkataba mpya wa mahitaji anayoyataka yeye.

Awali kulikuwa na taarifa kuwa nyota huyo tayari amemalizana na viongozi wake na uwenda akasaini mkataba mpya huku pia Yanga wakihusishwa kumtaka, uongozi wa Simba umeamua kumbananisha Chama na kumtaka kukubali masharti yao ikiwamo dau walilomwandalia ili wampe mkataba mpya.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kama mchezaji huyo hatakubali masharti hayo, uongozi umempa uhuru wa kuondoka.

“Kiukweli Chama bado hajasaini na mkataba wake nadhani umebaki siku chache sana, kulikuwa na mvutano ndani ya uongozi kuamua kama apewe mkataba mpya au waachane naye, sasa wamempa masharti ambayo kama atakubaliana nayo msimu ujao ataendelea kuichezea Simba,

“lakini bado hajasaini mkataba mpya, mashabiki wajiandae wanaweza wasimwone kwenye timu msimu ujao,” kilisema chanzo chetu ndani ya klabu hiyo bila kutaja kwa ndani masharti hayo.

Aidha, alisema uongozi unakijenga upya kikosi cha timu hiyo ili kurejesha makali yao lakini wanataka kubaki na wachezaji watakaojitoa kwa ajili ya timu na hawatakuwa na usumbufu muda wote.

“Moja ya mambo yanayotajwa kutuangusha msimu ulioisha ni wachezaji kutojituma, hawajitoi kweli kwa ajili ya timu, sasa tunataka wachezaji watakaoipigania kweli jezi ya Simba, ndio maana unaona mchezaji kama Mzamiru (Yassin) ameongezewa mkataba kwa sababu ni mmoja wa wachezaji waliokuwa wakijituma,” kilisema chanzo hicho.

Mbali na Mzamiru, Simba pia imetangaza kumwongezea mkataba beki Israel Patrick, Kibu Denis na Shomari Kapombe kuendelea kuitumikia timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu na michuano ya Kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika hatua nyingine, kiungo mshambuliaji raia wa Zambia, Joshua Mutale ambaye inaelezwa amesaini mkataba wa miaka mitatu kuitumikia timu hiyo, amewasili nchini juzi usiku.

Kiungo huyo aliyekuwa akiichezea klabu ya Power Dynamos ya nchini humo, msimu ujao atavaa jezi nyekundu kuitumikia timu hiyo ya Msimbazi.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YA SOKALEO, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here